HATIMAYE AMEOLEWA.
Kwa miaka zaidi ya kenda, urafiki tuliukoleza
Japo mbali nikaenda, pesa kuitafuta Muheza
Mupenzi alijilinda, nami penzi nikatunza
Leo nalia mwenyewe, hatimaye ameolewa
Ahadi tulitukuza, penzi tusije livunja
Maneno yake yalinikuza, kama samaki alinikunja
Moyo huba alinuiza, Muheza buzi sikuonja
Leo nalia mwenyewe, hatimaye ameolewa
Simu na jumbe mahabuba, zilinipata si haba
Hata sikuwaza suluba, kwa kazi zilizonikaba
Nami moyo ulinijaba, nikamwekeza hadi baba
Leo nalia mwenyewe, hatimaye ameolewa.
Mara wiki ikakatika, mupenzi hapatikani
Moyo nikajipa rika, labda simu matatani
Hata mwezi ukavunjika, Sina taarifa abadani
Leo nalia mwenyewe, hatimaye ameolewa
Nikafuata ushauri, kwa wahenga mashuhuri
Nipate vipi saburi, wa moyo sinaye habari
Baba kasema ni nzuri, kama nikipanga safari
Leo nalia mwenyewe, hatimaye ameolewa
Mwaka ulofata julai, nikarudi Shambarai
Huku najipa tumai, nenda posa wangu Nai
Furaha isiyokinai, kwa moyo wangu jinai
Leo nalia mwenyewe, hatimaye ameolewa.
Nikafika Kwao nyumbani, kwa furaha nikapokewa
Moyo ukajawa amani, langu tunda nitapewa
Nikatoa ya moyoni, kadiri nilivyojaliwa
Leo nalia mwenyewe, hatimaye ameolewa
Babaye kameza mate, sautiye itoke yote
Mwanangu sikiza yote, cha mtu usikiokote
Nai kashenda fungate, na mumewe wa Katote
Leo nalia mwenyewe, hatimaye ameolewa
baraka ngeleja
0756775148