MAUMIVU
Sili wala silali, ninakesha kama bundi
Umenichoma msumari, haoung'oki hata kwa fundi
Najua waona fahari, vicheko vyakutoka sundi
Maumivu ndo jina langu, nipe pole salamu yangu
Moyo wangu bado una jambo, nisikize mpenzi wangu
Kwako nishanasha chambo, usisulubu mtima wangu
Wengi wamekupa ulimbo, wakunase UA langu
Maumivu ndo jina langu, nipe pole salamu yangu.
Mangapi niliyapuuza, yalosemwa juu yako
Leo mambo wayakuza, eti mie sio taipu yako
Na vita unaitangaza, ama zangu ama zako
Maumivu ndo jina langu, nipe pole salamu yangu.
Kupenda hisani ya moyo, usiniumize mwenzio
Hata fukara haki ninayo, rudi unitulize mwenzio
Wakupao pesa wachoyo, wa penzi zaidi ya kileo
Maumivu ndo jina langu, nipe pole salamu yangu
Nauguza kidonda changu, unanitesa mpenzi wangu
Hakuna raha tena kwangu, ebu tazama machozi yangu
Vingi ulinizoesha wangu, chonde rudi hima kwangu
Maumivu ndo jina langu, nipe pole salamu yangu.
Ona watoto wanalia, subira imewaishia
Majirani walokuzoea, kutwa kuniulizia
Hivi kweli umeamua, pesa chanzo ukakimbia
Maumivu ndo jina langu, nipe pole salamu yangu.
Moyo umejaa imani, utarejea kwangu mpenzi
Tamaa zisikurubuni, U mbali nani ntamuenzi?
Pesa na vyote duniani, ni baraka za Mwenyezi.
Maumivu ndo jina langu, nipe pole salamu yangu.
Writer: baraka ngeleja
0756775148
Date: 16 July 2017.