Skip to main content

ETI KISA UMEUMBIKA!!

ETI KISA UMEUMBIKA!
NGELEJA©UPP

Rabi sinipe mapenzi, sijapata wa kuyaenzi
Bora n'zidishie tenzi, neleze hizi simanzi
Liko wapi lile penzi, uloapa utalienzi
Namba nane yako figa, moyoni mwangu ni mwiba.

Sote tulitii kiapo, maisha yangu ni yako
Hata popote tuendapo, u mlinzi nami ni wako
Hani ulipo mi nipo, ilikua ahadi yako
Namba nane yako figa, moyoni mwangu ni mwiba

Miezi kenda yapita, mke hujanipa tunda
Ndani warudi saa sita, hii tabia yanishinda
N'kihoji wakunja ndita, eti mi si wa kukulinda
Namba nane yako figa, moyoni mwangu ni mwiba

Unapenda vitu ghari, pesa magari swadakta
Unasema we mzuri, vigogo wengi wadata
Wajipuliza uturi, na waenda kula bata
Namba nane yako figa, moyoni mwangu ni mwiba

Pombe wanywa nyakanyaka, nusu uchi wavaa
Mwili watoa sadaka, wala huogopi zinaa
Sio mabosi si vilaka, wote umewapa ridhaa
Namba nane yako figa, moyoni mwangu ni mwiba.

Wamekuhonga na gali, sasa na ndani hulali
Ndoa wachezea kamali, Kwa mora dua nasali
Kama sikuwa rijali, ungesema wangu mwali
Namba nane yako figa, moyoni mwangu ni mwiba.

Kesho natoa talaka, unachie moyo wangu
Yanishinda yako hulka, haliwi na mmoja changu
Nasubilia labuka, anipe halali yangu
Namba nane yako figa, moyoni mwangu ni mwiba.

0756775148

Popular posts from this blog

Curriculum Vitae (C. V)

Jana nilifika katika kituo kimoja cha afya na katika Harakati za hapaaaa na pale, nikiwa nimekaa kwenye benchi ili nipumzike kidogo. Nikiwa pale wakatokea wauguzi wawili nao wakakaa karibu yangu na wakaanza kuzungumza. Mmoja akamwambia mwenzake juu ya changamoto za ajira na jinsi alivyojitahidi kutafuta nafasi hata za kujitolea bila kufanikiwa, na yule mwenzake nae akamwambia jinsi alivyopambana mpaka kupata nafasi hiyo japo wanalipwa ila bado ni posho kidogo sana. Sasa, katika mazungumzo yao mwanzoni hayakunihusu japokuwa niliyasikiliza Si unajua tena sikio halina mlango lakini walifikia kipindi wakanishirikisha kwa namna moja ama nyingine hasa walipoanza kujadili vikwazo walivyokutana navyo. Ni vikwazo vingi ila hivi viwili vitakuhusu hata wewe pia. Wakisema cha kwanza ni kuandika barua ya kuomba ajira ama kujitolea na ilitakuwa iandikwe kwa lugha ya kiigereza na kingine ni kuandaa wasifu binafsi (c.v) inayoonesha mtiririko mzuri wa taarifa zako. Hapo sasa wakanishirikisha. Ngoja ...